Dodoma, Tanzania, Mei 31, 2023— IFC leo imezindua Anaweza: ambao ni mpango mpana wa kuwawezesha wanawake wengi zaidi katika nyanja za uchumi nchini Tanzania ili waweze kupata fedha, kushika nyadhifa za uongozi katika sekta binafsi, na kuanzisha au kukuza biashara,kikiwemo kilimo.
Mpango huu wa ushauri wa miaka mitano una thamani ya dola milioni 10 ukiwa na malengo matatu: Kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa wanawake na ushiriki wao katika uongozi, kuongeza idadi ya wanawake wafanyabiashara na upatikanaji wa huduma za kifedha na zisizo za kifedha kwa ajili ya biashara zinazomilikiwa na wanawake, na kuimarisha biashara za wanawake ziweze kuongeza uzalishaji wa mtaji na kupata masoko katika sekta muhimu kama vile biashara ya kilimo, viwanda, huduma za kidijitali na utalii.
Ili kufikia malengo haya, IFC itashirikiana na wafanyabiashara wa Tanzania ili kukuza uwekezaji kwa wanawake kama viongozi na wafanyakazi ili kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi na kwenye bodi. Mpango huo pia utashirikisha washirika kutoka sekta ya umma na binafsi katika kuandaa huduma za kifedha na zisizo za kifedha zinazowalenga wanawake walioko katika biashara na kukuza shughuli zinazoongeza vyanzo vya fedha kutoka kwa wanawake wajasiriamali.
Mpango huu wa IFC unaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050, Sera ya Kitaifa ya Jinsia na Mkakati wake, na dhamira za serikali ya Tanzania katika kuleta usawa (
Tanzania Development Vision 2025, the National Five Year Development Plan III (2021/22-2025/26), Zanzibar Development Vision 2050, the National Gender Policy and its Strategy, and the Tanzania commitments on Generation Equality), na haya yote yameeleza hatua mbalimbali za kuimarisha thamani ya rasilimali watu kwa kulenga zaidi kuwawezesha wanawake na kuleta usawa wa kijinsia.
"Wanawake wanaweza kuwa injini ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Kuwawezesha wanawake kuchukua jukumu kubwa la kukuza uchumi kutawawezesha kuwa na maisha bora zaidi kwa watu binafsi na familia zao. Tutashirikiana na wabia wetu kutoka sekta ya umma na binafsi ili kufanikisha upatikanaji wa fursa zaidi za kuwajumuisha wanawake zaidi katika uchumi wa Tanzania," alisema Jumoke Jagun-Dokunmu, Mkurugenzi wa IFC Kanda ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Tathmini ya Benki ya Dunia kuhusu hali ya Jinsia Tanzania ya mwaka 2022, Tanzania imepiga hatua katika kuongeza usawa wa kijinsia, na serikali imefanya jitihada za kukabiliana na ukosefu wa usawa wa kijinsia katika nyanja zote za maisha ya wanawake lakini bado kuna mapungufu kadhaa. Programu hii ya IFC ya Anaweza: inalenga kushughulikia mengi ya mapungufu haya.
Kwa mfano, ushiriki wa nguvu kazi ya wanawake nchini Tanzania unakadiriwa kufikia asilimia 80, lakini nguvu kazi hii iko zaidi katika kilimo kisicho rasmi ambapo wanawake ni wengi zaidi na wanamiliki mashamba madogo yasiyo na tija. Wakati huo huo, asilimia 75 ya biashara zinazomilikiwa na wanawake nchini Tanzania haziwezi kupata mitaji kutoka kwenye taasisi za fedha kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa dhamana au uelewa mdogo kuhusu huduma za kifedha zinazotolewa.
Kwa mujibu wa data za Boardroom Africa kuhusu Tofauti za Jinsia, wanawake walioko kwenye uongozi kwenye sekta binafsi ni wachache sana, kwani ni asilimia 19 pekee ya wanawake wako kwenye nafasi za ujumbe wa bodi za wakurugenzi wa kampuni zilizoorodheshwa kwenye masoko ya mitaji. Katika nafasi za utendaji, pengo la nafasi kwa wanawake ni kubwa zaidi huku wanawake wakichukua asilimia 4 tu ya Maofisa Watendaji wa kampuni zilizoorodheshwa kwenye masoko ya mitaji.
Kupunguza usawa wa kijinsia ni nguzo muhimu ya kazi ya kijinsia ya IFC kote Afrika, inayohusisha uwekezaji na ushauri, utafiti wa kuangazia hali ya kibiashara kwa kuziba mapengo ya kijinsia, na ushirikiano wa kimataifa na nchi mahususi. Shughuli za IFC zinalenga katika kuboresha upatikanaji wa fursa za wanawake katika ujasiriamali, ajira, bima, uongozi wa mashirika, na uchumi wa kidijitali.
Kuhusu IFC
IFC— ni taasisi ya Benki ya Dunia — ni taasisi kubwa ya kimaendeleo duniani inayojielekeza katika kusaidia kujengea uwezo sekta binafsi. Tunafanya kazi kwenye nchi zaidi ya 100, tukilenga kutumia mitaji yetu, uzoefu, na ushawishi wetu katika kutengeneza masoko na fursa mbalimbali kwa nchi zinazoendelea. Kwa mwaka wa fedha wa 2022, IFC ilipanga kutumia dola bilioni 32.8 kwa ajili ya kampuni binafsi na taasisi za fedha kwenye nchi zinazoendelea, kuweza kutumia sekta binafsi kutokomeza umaskini na kukuza ukuaji wa uchumi wa nchi huku zikiwa zinakabiliana na athari za majanga mbalimbali yanyotokea duniani. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti yetu
www.ifc.org.
Fuatilia kwa karibu